06 February 2012

Mgomo: Serikali yawalaumu walimu

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Mwantumu Mahiza amewatupia lawama wakuu wa shule kutokana na migogoro mingi inayotokea katika shule mbalimbali za sekondari na kusema mingi huchangiwa na walimu kushindwa kuwasoma wanafunzi.


Pia ametoa agizo kwa wakuu wa shule kutoruhusu migogoro hiyo kwa sasa na kuongeza kuwa atawachukulia hatua za kinadhamu wakuu wa shule zitakazofanya vurugu ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.

Bi.Mwantumu alisema hayo hivi karibuni Dar es Salaam katika shule ya sekondari ya Wasichana Jangwani, wakati akifungua kikao cha Umoja wa Wakuu wa Shule Tanzania Bara (TAHOSSA) chenye lengo la kujadili kiini cha migogoro shuleni.

Bi. Mwantumu alisema viongozi wa serikali wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenda kusuluhisha migomo shuleni na machafuko ambayo yamekuwa yakisababisha hasara kwa serikali na shule kwa ujumla licha ya kuwepo wakuu wa shule ambao wamepewa dhamana na wizara ya kuongoza shule hizo.

"Napata hofu kuwa kuna mahali tunakosea katika uongozi shuleni, mmeshindwa waoi kiasi cha kusababisha wanafunzi kugoma na kufanya vurugu au mmeshindwa kuwasoma wanafunzi wenu,  sitaungana nanyi na nitakuwa mkali kwa malalamiko yoyote.

Baada ya kikao cha leo sipendi kusikia fujo katika shule yoyote na endapo itatokea tutawachukulia hatua wakuu wa shule ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi, sipendi kusikia kelele tena bali tukabiliane na changamoto ya upungufu wa walimu, maabara na ukosefu wa vifaa vya kufundishia", alisema Bi. Mahiza.

Naibu Waziri huyo aliwataka wakuu hao wa shule kuwajibika katika maeneo yao ya kazi na kuwashirikisha wanafunzi wao katika maamuzi na mabadiliko katika maendeleo ya shule ikiwa ni pamoja na kuwapa taarifa mbalimbali za mambo muhimu yakiwemo matumizi sahihi ya fedha za shule.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amesikitishwa na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu akitolea mfano wanafunzi walioambiwa kunawa maji ya kinyesi mkoani Kilimanjaro ikiwa ni pamoja na kutumikishwa kazi ngumu.

"Wakuu wa shule tulieni katika vituo vyenu vya kazi mnakuwa wapi hadi wanafunzi wanaambiwa kunawa kinyesi, wengine wanatumikishwa kazi za mashambani kwa muda mrefu mambo hayo yote yakifanyiwa marekebisho yatasaidia kuondoa migogoro", alisema naibu waziri huyo.

  

No comments:

Post a Comment