03 December 2013

KAMPUNI ZASHAURIWA KUHUSU AFYA ZA WAFANYAKAZI



 Kampuni na taasisi mbalimbali nchini zimeshauriwa kujua hali ya afya za wafanyakazi kwa sababu itasaidia pia kuongeza mchango wao uzalishaji katika sehemu zao za kazi, anaripoti Mwandishi Wetu.

Kauli hii ilitolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam (RAS),Teresia Mbando wakati wa maadhimisho ya Siku ya UkimwiDuniani katika makao makuu ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Bi.Mbando alisema huku suala la maambukuzi ya VVU / Ukimwi yakiwa yanaongezeka, ni muhimu kwa kampuni na taasisi kuchukua hatua ya kujua hali ya afya za wafanyakazi wake akisema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kutekeleza harakati na mpango wa serikali wa mapambano dhidi ya Ukimwi.
Alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutokomeza ugonjwa huo na kusema kuwa kwa 'kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi ya " kufikia asilimia sifuri katika maambukizi mapya,unyanyapaa na idadi ya vifo vinavyotokana na Ukimwi, inaonyesha kwamba juhudi zaidi zimeelekezwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Mbando aliipongeza TBL kwa kuweka mbele suala la afya ya wafanyakazi wake na kutoa wito kwa kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano huo, kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza kwa kiasi kiwango kikubwa cha maambukizi mapya.
Kwa upande wake, Meneja Rasilimali wa TBL, David Magesa alisema tokea mwaka 1990, kampuni hiyo ilikuwa na mpango ambao unawawezesha kupata huduma ya upimaji wa hiari na Ushauri nasaha.
Magesa alisema pia hadi sasa asilimia 80 ya wafanyakazi wa TBL wanajua hali ya afya zao, akibainisha kuwa mpango huu unafanyika kutokana na kuungwa mkono na utawala wa kampuni hiyo.
"Mbali na upimaji wa hiari na Ushauri nasaha, kampuni kupitia kliniki yake ambayo imejitosheleza inatoa bure dawa za kurefusha maisha (ARVs) na mpango huo pia unashirikisha zaidi ya asilimia 40 ya wanafamilia wa wafanyakazi," alisema.
Aidha, Magesa alisema kupitia programu hiyo wameweza kupunguza idadi ya vifo kwa asilimia 99.9 pamoja na kupunguza kesi za maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STDs) na kuongezea kuwa programu hiyo imekuwa ya manufaa makubwa si tu klwa wafanyakazi bali hata wasio wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Mbali na hayo alisema kuwa kampuni hiyo hadi sasa ina waelimishaji rika 116 ambao wanashiriki katika kutoa ushauri kwa wafanyakazi wenzao ili kuwafanya wawe na ufahamu katika kutambua umuhimu wa kujua hali ya afya zao.


1 comment: