04 December 2013

KILI STARS 'MTOTO HATUMWI SOKONI LEO'



 Na Mwandishi Wetu, Nairobi
Timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), leo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Burundi katika mechi ya michuano ya Chalenji inayofanyika jijini hapa, ikiwa inawania pointi tatu muhimu ili kujiweka vizuri kucheza robo fainali ya mashindano hayo.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen anayesaidiwa na Sylivester Marsh, itacheza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Nakuru nje kidogo ya jiji la Nairobi, saa 8 mchana ambapo itaamua timu ipi itakayosonga mbele.
Akizungumzia mchezo huo, Poulsen alisema kikosi chake amekiandaa kwa ajili ya ushindani ili kuhakikisha inashinda mechi hiyo na kusonga mbele.Poulsen alisema wamefanya mazoezi ya nguvu, kwa ajili ya kutoa upinzani kwa Burundi ambayo nayo inahitaji ushindi kwa udi na uvumba.
Alisema, anatarajia kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa Burundi inacheza vizuri na ina kikosi kizuri chenye kuleta changamoto kwa wapinzani wao.Kocha huyo raia wa Denmark alisema wana uhakika katika mechi ya leo wachezaji wake watajituma ili kushinda na kuwapa matumaini Watanzania.
Alisema pamoja na michezo mingine ya michuano hii itatoa nafasi kwa wachezaji wake vijana kuonesha uwezo wao."Ninatarajia wachezaji wangu watapata wakati mgumu katika mchezo wa leo kutokana na uwanja utakaotumika ambao una nyasi za kawaida, kwa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya mazoezi kwenye uwanja wenye nyasi bandia," alisema.
Katika mchezo wa leo, Kili Stars itaongezewa nguvu na washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).


2 comments: